Thursday 11 February 2010

Jerry Murro.

MWANDISHI wa habari ambaye pia ni mtangazaji wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC), Jerry Muro, amepandishwa kizimbani kujibu mashitaka mawili likiwemo la kuomba rushwa ya sh milioni 10/=. Muro amepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi, Kisutu, Dar es Salaam, pamoja na wanaodaiwa kuwa watuhumiwa sugu wa utapeli.
Muro ni mshitakiwa wa kwanza katika kesi hiyo, washitakiwa wenzake wawili wanakabiliwa na mashitaka matatu likiwemo linalowakabili wote la kuomba rushwa ya Sh milioni 10 kwa aliyekuwa Mhazini wa Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo, Michael Karoli. Washitakiwa wengine ni Edmund Kapama na Deogratias Mgasa.
Wakili wa Serikali, Boniface Stancilaus, na Wakili wa Taasisi ya Kuzuia na Kuapambana na Rushwa (TAKUKURU) Benny Lincolin, wamedai mahakamani kuwa, Januari mwaka huu washitakiwa hao na wengine ambao bado hawajakamatwa walipanga njama za kutenda kosa. Kwa mujibu wa mawakili hao, Januari 29 mwaka huu, Muro na wenzake walimuomba Karoli rushwa ya sh milioni 10. Mahakama imeelezwa kuwa, washitakiwa hao waliomba rushwa hiyo katika hoteli ya Sea Cliff, iliyopo katika ufukwe wa Bahari ya Hindi, Dar es Salaam. Mawakili hao wamesema, washitakiwa hao walikiuka kifungu cha 15(1) cha sheria ya kuzuia na kupambana na rishwa cha mwaka 2007. Katika mashitaka ya tatu, ilidaiwa mahakamani kuwa, Januari 29 mwaka huu, katika hoteli ya Sea Cliff, Kapama na Mgasa, walimdanganya Karoli kuwa wao ni maofisa wa Takukuru.
Washitakiwa hao wamekana mashitaka, upande wa mashitaka uliiomba mahakama iwanyime dhamana kwa madai kuwa wanaweza kuharibu upelelezi. Upande wa mashitaka pia ulidai kuwa, mshitakiwa wa pili na wa tatu waliwahi kuhukumiwa miaka mitatu kutokana na makosa ya utapeli. Hakimu Mkazi, Gabriel Mirumbe, alikataa ombi hilo kwa kuwa upande wa mashitaka umeshindwa kuwasilisha vielelezo kuhusu hukumu hiyo. Hakimu huyo alitoa masharti ya dhamana kwa kuwataka washitakiwa wapeleke wadhamini awili watakaosaini hati ya dhamana ya Sh milioni tano kila mmoja. Muro na Kapama walitimiza masharti hayo, wapo nje kwa dhamana, Mgasa amerudishwa rumande, kesi hiyo itatajwa tena Februari 12, mwaka huu.

Polisi walimkamata Muro, Januari 31 mwaka huu mchana, katika hoteli ya City Garden, Dar es Salaam, akidaiwa kutaka apewe rushwa ya Sh milioni 10.

source by
HABARI LEO

No comments:

Post a Comment